Siku
From Wikipedia
Siku ni muda wa wakati wa masaa 24 ambamo tunaona vipindi viwili vya mwanga wa mchana na giza ya usiku.
[edit] Mchana na usiku
Mabadiliko haya ya mchana na usiku husabibishwa na mzunguko wa dunia kwenye kipenyo chake. Upande wa dunia unaotazama jua unaona mwanga wa mchana lakini upande mwingine usiotazama jua uko gizani.
Sisi pamoja na mahali petu tunapokaa duniani tunazunguka kipenyo cha dunia. Mara tunatazama upande penye mwanga wa jua ni mchana; mara tunaangalia giza ya angani na kuona usiku.
[edit] Muda wa siku
Mzunguko huo una muda wa nukta (sekondi) 86,400 au masaa 24.
Kwa sababu muda wa mzunguko haulingani kamili na kipimo cha sekondi kuna siku ndefu au fupi zinazopatikana kwa kuingiza au kupunguza nukta moja kufuatana na azimio ya wataalamu wa wakati. Hii haina umhimu wowote katika maisha ya kila siku lakini inapaswa kuangaliwa pale ambako saa kamili sana ya kiatomi hutumiwa.
[edit] Siku na mwaka
Dunia pamoja na kuzunguka kwenye kipenyo chake inafuata pia mwendo wa kuzunguka jua. Ikikamilika mwendo huu mwaka umekamilika. Muda wa mwaka haulingani kamili na mizunguko ya dunia kwenye kipenyo chake. Hii ni sababu ya kalenda ya Gregori kuwa na mwaka wa kawaida wa siku 365 na kila mwaka wa nne kuwa na siku 366.