Simba Wanyika
From Wikipedia
Simba Wanyika ni bendi ya muziki iliyokuwa na makazi yake nchini Kenya. Bendi hii ilianzishwa mwaka 1971 na ndugu wawili Watanzania, Wilson Kinyonga na George Kinyonga, na ilivunjika mwaka 1994. Simba Wanyika ni moja ya bendi kubwa zitakazokumbukwa na kuheshimiwa daima katika duru za muziki Afrika Mashariki na Kati. Bendi nyingine kubwa katika historia ya muziki nchini Kenya na Afrika, Les Wanyika na Super Wanyika Stars,ziliundwa na wanamuziki waliopitia Simba Wanyika. Nyimbo zao zilirembwa na magitaa yaliyopigwa kwa ustadi uliotokana na staili ya mpiga gitaa wa Soukous, Dr. Nico.
Wilson Kinyonga na George Kinyonga walianza muziki nchini Tanzania, katika mji wa Tanga walipojiunga na kundi la Jamhuri Jazz Band hapo mwaka 1966. Mwaka 1970 walihamia mjini Arusha na kuanzisha kundi la Arusha Jazz na ndugu yao mwingine, William Kinyonga. Wakati huo wanamuziki wa nchi za Kenya na Tanzania walikuwa wakitembelea nchi hizi mbili mara kwa mara na kwa urahisi. Hapo mwaka 1971 Wilson na George Kinyonga walihamia nchini Kenya na kuanzisha Simba Wanyika. Bendi hii ilikuwa ikipiga kwenye baa na vilabu vya usiku nchini Kenya ambapo iliweza kuwa na mashabiki wengi na nyimbo zinazopendwa hadi leo.
Bendi ya Simba Wanyika ilisambaratika mwishoni mwa miaka ya 70 kutokana na mpiga gitaa la ridhimu wa bendi hiyo, Omar Shabani (Profesa Omar), kuhama na baadhi ya wanamuziki wa kundi hilo na kuanzisha kundi la Les Wanyika. Mwkaa 1980, George Kinyonga naye aliondoka Simba Wanyika na baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo na kuanzisha kundi la Orchestra Jobiso. Lakini baadaye alirudi Simba Wanyika huku akiendelea na bendi ya Orchestra Jobiso. Simba Wanyika baadaye ilibadili jina lake na kuitwa Simba Wanyika Original ili kujitofautisha na na bendi za Les Wanyika na Super Wanyika Stars.
Simba Wanyika ilipata umaarufu tena katikati ya miaka ya 80 kwa kutoa upya nyimbo zake na kufanya ziara ya Ulaya mwaka 1989. Simba Wanyika ilivunjika rasmi mwaka 1994.